Alhamisi 2 Oktoba 2025 - 07:05
Wajibu na Majukumu Maalum ya Wenye kusubiri

Hawza / Katika zama hizi si haba watu ambao, kwa sababu mbalimbali, hawawezi kuvumilia katika kumuamini Imam aliye ghaibu na kumkumbuka yeye. Kwa kuwa moja ya mafundisho muhimu ya dini ni subira juu ya matatizo na misiba, ni wajibu katika kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote kuwa na uvumilivu mbele ya changamoto hizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Wajibu maalum ni yale majukumu ambayo kwa namna moja au nyingine yanahusiana na ghaiba ya Imam Mahdi (ajtf). Majukumu hayo ni kama:

1. Urafiki na marafiki na uadui na maadui wa Imam Mahdi (ajtf)

Katika riwaya nyingi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kumesisitizwa juu ya mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s.) na uadui dhidi ya maadui zao. Hili ni la zama zote; lakini baadhi ya riwaya zimesisitiza kwa namna mahsusi juu ya upendo kwa marafiki wa Imam Mahdi na uadui kwa maadui zake.

Imam Muhammad al-Baqir (a.s.) amepokea kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.):

«طُوبی لِمَنْ اَدْرَکَ قائِمَ اَهْلِ بَیتی وَهُوَ یأتَمُّ بِهِ فی غَیْبَتِهِ قَبْلَ قِیامِهِ وَیَتَوَلّی اَوْلِیاءَهُ وَیُعادِی اَعْداءَهُ، ذلِکَ مِنْ رُفَقایی وَ ذَوِی مَوَدَّتی وَاَکْرَمُ اُمَّتی عَلَی یَوْمَ القِیامَةِ.»

“Hongera kwa yule atakayeupata wakati wa Qā’im wa Ahlul-Bayt wangu, na katika ghaiba yake kabla ya kudhihiri kwake, akawa anamfuata, akiwapenda marafiki zake na kuwachukia maadui zake. Mtu huyo atakuwa ni miongoni mwa wenzangu na wapendwa wangu na ni wa heshima kubwa zaidi miongoni mwa umma wangu Siku ya Kiyama.”

(Kamal al-Din wa Tamam al-Ni‘mah, j. 1, uk. 286)

2. Subira juu ya magumu ya zama za ghaiba

Katika zama hizi, watu wengi hawawezi kuvumilia kumwamini Imam aliye ghaibu. Moja ya mafundisho ya dini ni subira juu ya mitihani na matatizo. Hivyo basi, ni wajibu mkubwa zaidi katika kipindi cha ghaiba.

Abdullah ibn Sinan amepokea kutoka kwa Imam Ja‘far al-Sadiq (a.s.) kwamba Mtume (s.a.w.w.) alisema:

«سَیَأْتِی قَوْمٌ مِنْ بَعْدِکُمْ الرَّجُلُ الْوَاحِدُ مِنْهُمْ لَهُ أَجْرُ خَمْسِینَ مِنْکُمْ. قَالُوا: یَا رَسُولَ اللَّهِ نَحْنُ کُنَّا مَعَکَ بِبَدْرٍ وَ أُحُدٍ وَ حُنَیْنٍ وَ نَزَلَ فِینَا الْقُرْآنُ. فَقَالَ: إِنَّکُمْ لَوْ تَحْمِلُونَ لِمَا حُمِّلُوا لَمْ تَصْبِرُوا صَبْرَهُمْ.»

“Baada ya zama zenu, watu watakuja, na kila mmoja wao atapata ujira sawa na watu hamsini kati yenu.” Wakasema: “Ewe Mtume wa Mungu! Sisi tulipigana pamoja nawe katika Badr, Uhud na Hunayn, na Qur’an imeteremshwa kutuhusu!” Akasema: “Lau mngebebeshwa yale waliyobebeshwa wao, msingevumilia uvumilivu wao.”

(Shaykh al-Tusi, Kitāb al-Ghaybah, uk. 456)

Imam Husayn ibn Ali (a.s.) pia alisema:

«اِنَّ الصَّابِرَ فِی غَیبَتِهِ عَلَی الاَذی وَالتَّکْذِیبِ بِمَنزِلَةِ المُجاهِدِ بِالسَّیْفِ بَیْنَ یَدَی رَسُولِ اللَّهِ صلی‌الله‌علیه‌وآله‌وسلم.»

“Yule mwenye subira juu ya maudhi na kukanushwa katika zama za ghaiba yake, ni sawa na mjahid anayepigana kwa upanga mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.).”

(Kamal al-Din wa Tamam al-Ni‘mah, j. 1, uk. 317)

3. Dua kwa ajili ya Faraja ya Imam Mahdi (ajtf)

Dua na maombi vina nafasi kubwa katika utamaduni wa Kiislamu. Miongoni mwa dua ni kuomba kuondolewa kwa matatizo ya wanadamu wote. Kwa mtazamo wa Shia, jambo hili halitatimia kikamilifu ila kwa kudhihiri kwa Imam Mahdi, ambaye ataiangaza dunia kwa nuru yake. Ndiyo maana riwaya nyingi zimesisitiza kuomb dua ya kuharakishwa kwa faraja yake.

Imam Mahdi (ajtf) mwenyewe katika sehemu ya moja ya tawqi‘ yake alisema:

«وَاَکثِرُوا الدُّعاء بِتَعجیلِ الفَرَجِ.»

“Kithirisheni dua kwa ajili ya kuharakishwa kwa faraja.”

(Kamal al-Din wa Tamam al-Ni‘mah, j. 2, uk. 483)

Marehemu Ayatullah Ali Pehlavani Tehrani (1926–2004), anayejulikana kama Ali Saadatparvar, arifu wa Kishia ambaye alikamilisha hatua za suluk chini ya Ayatullah Allamah Sayyid Muhammad Husayn Tabataba’i (mwandishi wa Tafsīr al-Mīzān), amesema kuhusu jambo hili:

“Bila shaka kila mtu anajua kuwa kusisitiza kwa Imamu juu ya kuomba na kusoma dua, lengo siyo tu kutamka maneno kwa ulimi na kuyasoma kwa kurudia-rudia; ingawa kusoma dua yenyewe kuna malipo maalumu. Bali makusudiwa ni kuwa na uelekevu wa daima wa moyo katika maana na dhati ya dua hii, na kuelewa kuwa katika kipindi cha ghaiba, jambo la dini, kushikamana na dini na kuwa na imani sahihi juu ya ghaiba na uongozi wa Imamu ni jambo gumu ambalo halitoweza kufanywa ila na mtu mwenye yakini na ustahimilivu wa kweli.”

(Zuhur-e-Nūr, uk. 103)

4. Daima kuwa maandalizi

Miongoni mwa majukumu muhimu zaidi katika zama za ghaiba ni kuwa katika hali ya maandalizi ya daima na ya kweli, kuhusiana na hili, kuna riwaya nyingi.

Imam Bāqir (as) akisimulia Aya hii:

«اصْبِرُوا وَ صابِرُوا وَ رابِطُوا؛ 

"Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho" [Qur’ān 3:200], alisema:

«اصْبِرُوا عَلَی أَدَاءِ الْفَرَائِضِ وَ صَابِرُوا عَدُوَّکُمْ وَ رَابِطُوا إِمَامَکُمْ المنتظر.»

“Shikamaneni juu ya utekelezaji wa wajibu, saidianeni dhidi ya adui wenu, na msimame tayari kwa ajili ya Imamu wenu anayengojewa.”

(Nu‘mani, al-Ghaybah, uk. 199)

Kinyume na dhana ya baadhi ya watu waliotafsiri neno «رابطوا» kama kuwasiliana au kukutana na Imamu, neno hili kimsingi linamaanisha kuwa katika hali ya utayari kwa ajili ya mapambano.

(Lisan al-‘Arab, j. 7, uk. 303; Majma‘ al-Bahrayn, j. 4, uk. 248)

5. Kuheshimu jina na kumbukumbu ya Imam

Miongoni mwa majukumu ya Shia kuhusu Imamu Mahdi (aj) katika zama hizi ni kuheshimu jina na kumbukumbu yake. Heshima hii ina sura nyingi: kuandaa vikao vya dua na ibada, shughuli za kielimu na kiutamaduni, mikusanyiko ya upekuzi na mijadala, pamoja na tafiti za kimsingi na zenye manufaa yote ni njia za kuenzi jina la Imam.

6. Kuhifadhi uhusiano na Wilaya

Kuhifadhi na kuimarisha kiunganishi cha moyoni na Imamu wa zama (aj) na kufanyia upya ahadi ya utii daima, ni miongoni mwa majukumu muhimu ya kila Shia anaesubiri katika kipindi cha ghaiba.

Imam Bāqir (as) kuhusu wale wanaobaki imara juu ya uongozi alisema:

«یَأْتِی عَلَی اَلنَّاسِ زَمَانٌ یَغِیبُ عَنْهُمْ إِمَامُهُمْ فَیَا طُوبَی لِلثَّابِتِینَ عَلَی أَمْرِنَا فِی ذَلِکَ اَلزَّمَانِ... فَأَنْتُمْ عِبَادِی وَ إِمَائِی حَقّاً... وَلَوْلاَکُمْ لَأَنْزَلْتُ عَلَیْهِمْ عَذَابِی.» 

“Utafika wakati ambapo watu watamkosa Imamu wao. Basi heri ni kwa wale watakaobaki thabiti juu ya jambo letu katika zama hizo! Malipo madogo zaidi watakayopata ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atawalingania na kusema: ‘Enyi waja wangu na vijakazi vyangu! Mmeamini katika siri yangu na mkasadikisha ghaiba yangu; basi furahini kwa malipo mema kutoka kwangu. Nyinyi kweli ni waja wangu na vijakazi wangu. Kutokana na nyinyi nakubali, na kutokana na nyinyi ninasamehe, na kwa ajili yenu nawanyeshea waja wangu mvua na kuondoa mitihani kutoka kwao. Na lau siyo nyinyi, ningewateremshia adhabu yangu.’”

(Kamal al-Din wa Tamam al-Ni‘mah, j. 1, uk. 330)

Utafiti huu unaendelea…

Imenukuliwa kutoka katika kitabu: «Darname Mahdaviyat» kilicho andikwa na "Khodā-Morād Salīmiyān", huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha